Monthly Archives: October, 2012

LIKIZO YA MKULIMA

Na Evaristo Haulle

 

Mvua lini yashuka, kwa malisho yasomea?

Ngorongoro wanavuka, Musoma wanyemelea

 Ili ilete fanaka, maziwa yatatomea

Likizo ya mkulima, lini itamfikia

 

Huku ng`ombe wamekufa, huku bei imeshuka

Malisho yake masafa, uvivu wamemvika

Amelilisha Taifa, Kitoweo bilashaka

Likizo ya mkulima, lini itamfikia

 

Januari ikifika, udongo umetifua

Palizi imemteka, mbolea inamfua

Kuvuna kwake kwashaka, hatayakosa mafua

Likizo ya mkulima, lini itamfikia

 

Mfuko mbolea laki, ruzuku eti apata

Mazao bei si haki, vipi likizo apata

Ubora wasoafiki, ni aje bei tapata

Likizo ya mkulima, lini itamfikia

 

Kila siku adumaa, wadai sio bunifu

Bei wanaiandaa, niaje kosa dhoofu

Mvua weka mataa, mavuno yasosadifu

Likizo ya mkulima, lini itamfikia

 

Wakamletea jambo, kufa kupona kilimo

Hajatulia na jambo, siasa ndio kilimo

Padepu weka kiwambo, utata sana kilimo

Likizo ya mkulima, lini itamfikia

 

Ikaja kilimo kwanza, utata waongozana

Na huyo elimu kwanza, sasa mbona mwabishana

Pataneni ninyi kwanza, kilimo sio bishana

Likizo ya mkulima, lini itamfikia

 

Zote ziliahidia, kilimo utimgongo

Huku wakishadadia, jembe mkono kisogo

Hapa nina shuhudia, pawalita nikigongo

Likizo ya mkulima, lini itamfikia

 

Asipovuna kwa wingi, wanamtaja mvivu

Atalimaje kwawingi, mwamtwika zana mbovu

Mwamtapeli kwa mengi, pembejeo zake mbovu

Likizo ya mkulima, lini itamfikia

 

Ataendaje likizo,kama hakuna surufu

Wamedhulumu nguvuzo, sasa wanakusanifu

Wanapoenda likizo kwa jasho lakihalifu

Likizo ya mkulima, lini itamfikia

 

Kwamuda amewalisha, sisi yetu ufisadi

Tangu bendera pandisha, hamsini imezidi

Laity haikutosha, mashamba twamfisadi

Likizo ya mkulima, lini itamfikia

 

Nani atajitolea, walau mfuta jasho

Ngonjera hatopokea, apate walau posho

Mapumziko pokea walau ampe josho

Likizo ya mkulima, lini itamfikia

 

Jua kwa mvua pigo, sasa mpe kiyoyozi

Kama uti wa mgongo, apate sasa pongezi

Ashiriki na mipango, awepia kielezi

Likizo ya mkulima, lini itamfikia

Advertisements

NAMBA ZAKO

Evaristo Haulle

Daudi jina mwangosi, sasa ninakuanika,
Kwa ugumu si wepesi, Jinalo linatukuka,
Kwa bomu tunaakisi, damuyo ilomwagika,
Damu daudi mwangosi, Haito mwagika bure.

Ya kwanza ni namba yako, Tanzania mwaka huu
Ya kwanza ni namba yako, miaka yote na huu
Ya mwandishi namba yako, kupata ushenzi huu
Damu daudi mwangosi, Haito mwagika bure.

Nne sita namba yako, jeshi kuua nchini
Tatu tisa namba yako, wa mwaka hu si mwakani
Mwandishi ni namba yako, kuuwa duniani
Damu daudi mwangosi, Haito mwagika bure.

Mbili saba namba yako, mwezi twataja julai,
Efu mbili namba yako, sita tunaijumui,
Siku hii namba yako, taufik wabilai,
Damu daudi mwangosi, Haito mwagika bure.

Myaka sita namba yako, twakuona luningani,
Sijachoka nambayako, ripoti chaneli teni,
Ni ya kwanza namba yako, Iringa kutubaini,
Damu daudi mwangosi, Haito mwagika bure.

Wakamia namba yako, wadhani unafaidi,
Saa nne, namba yako, kalamu isowazidi,
Watimiza namba yako, nyororo huko Mufindi,
Damu daudi mwangosi, Haito mwagika bure.

Thelathini namba yako, moja ndio januari,
Kuzaliwa namba yako, mia-kenda twakariri,
Saba-mbili namba yako, uhai ulikabiri,
Damu daudi mwangosi, Haito mwagika bure.

Mbona ndogo namba yako, miaka arobaini,
Washuruti namba yako, umri wako duniani,
Isitoshe namba yako, ukweli twaubaini,
Damu daudi mwangosi, Haito mwagika bure.

Na tatu ni namba yako, watoto ulowaacha
Mbili tisa namba yako, tarehe ulotuaga
Ishirini namba yako, kumi-mbili mwaka funga
Damu daudi mwangosi, Haito mwagika bure.

Kinyume cha Mambo

Mambo kinyume kinyume, wangwana nipe maana,

Njaa, shibe ni kinyume, hilo twalijua mana,

Nisiupige ukeme, Utata ninaunena,

Mambo kinyume kinyume, wangwana nipe maana

 

Hapa ni amri ya jiji, usitupe taka ovyo

Hata uwe mwovoshaji, samaki maji wa taka

Nashangaa hili jiji, hapo zimejaa taka

Mambo kinyume kinyume, wangwana nipe maana

 

Jeshi letu la polisi, usalama wa raia

Wasokosa mwafilisi, amani mwaigunia

Wake wamepokwa jasi, Risasi wa fyatulia

Mambo kinyume kinyume, wangwana nipe maana

 

Adui wa haki rushwa, fisini hakubaliki,

Mbele kamwe hutapishwa, kama chai haitoki,

Sheria imepindishwa, apewe asostahiki,

Mambo kinyume kinyume, wangwana nipe maana

 

Usifanye biashara, eneo limezuiwa,

Hapo waleta msara, kusimama pazuiwa,

Kusimama biashaara, hapo ndipo vinafanywa,

Mambo kinyume kinyume, wangwana nipe maana

 

Kwa kasi tunashindana, sheli mafuta kutia,

Hapa sigara hakuna, ndipo tunapovutia,

Dhibiti mwendo gongana, mwendo kasi tunatia,

Mambo kinyume kinyume, wangwana nipe maana

 

Wa viwango wakidai, chakula hiki salama

Ukweli usijidai, kukila kama mnuma

Wakisema hakifai, kinyume chake simama

Mambo kinyume kinyume, wangwana nipe maana

 

Mapato tunahitaji, bia sigara pitia

Viwanda tunavihiji, ulevi noma twalia

Siha njema twahitaji, John woka kupitia?

Mambo kinyume kinyume, wangwana nipe maana

 

Hapa gari maji safi, Nafuu la taka maji,

msamiati usafi, yaweje masafi maji,

manake nini usafi, si safi gari na maji,

Mambo kinyume kinyume, wangwana nipe maana

 

Kwanini haya yajili, jamii yenye mapepe,

Ukweli twaubadili, nyeusi iwe nyeupe,

Umakini si halali, kwetu vyote ni matope,

Mambo kinyume kinyume, wangwana nipe maana

JE MWAROBAINI WA FOLENI DAR ES SALAAM NI UPI ?

Nimeamua kujitokeza hapa na kuandika kwa lengo kuuliza tu sina majibu, najaribu kuuliza tu. Yeyote awaye najibu aweza jibu. Leo nimepita pande za jiji la Dar es Salaam kuona wengi wanafurahia na kusubiri kwa namna ya pekee mradi wa mabasi yaendayo kasi.
Katika hili mie sikuzote hofu yangu hayo magari yatapita wapi? Jibu rahisi kuna barabara maalumu zitajengwa. Kwa haraka ni jambo jema sana lakini msongamano huu jijini unatokana na magari yaliyopo kusafiri kwa mwendo mdogo? Kama ndivyo je tutayapeleka wapi magari yaliyopo? Bado majibu ya maswali haya sio magumu tutayanyima leseni ya kufanya kazi katikati ya jiji.
Je magari binafsi nayo yatazuiliwa? Je hayo magari yatapita katika mataa bila kusimama kama magari ya wagonjwa au msafara wa viongozi? Haya ni baadhi tu ya maswali yanayoweza ulizwa na yeyote na majibu yakawa rahisi.
Ukweli wa mambo ni kwamba hayo ni magumu ukilinganisha na hali ya jiji lenyewe. Kwa mtazamo wangu hapo tutakuwa tunahairisha tatizo lililopo. Kiufupi Dar es Salaam inatakiwa ijengwe upya kutokana na zaidi ya 75% ya jiji halijapangika. Hii inamaanisha kama tukihitaji kutatua tatizo lililopo sasa la msongamano tutalazimika kumpa Dr. Magufuli kazi ya bomoa bomoa ya sehemu kubwa ya makazi yaliyopo Dar es Salaam.
Tatizo la foleni Dar es Salaam kwa sasa linasababisha na mpango wenyewe wa barabara kama suala la msingi, Jambo la pili ni aina ya makutano na viunganishi vya barabara.
Nianze na aina ya viunganishi. Viunganishi ambavyo ni chanzo cha msongamano wa magari ni vile vinavyo fahamika kama mizunguko maarufu kama “ Round about” au “Keep Left” Mzunguko wa Msimbazi, mzunguko wa Sanamu ya Jasmini Posta na Mzunguko wa mnara wa saa maeneo ya stesheni ni mifano michache ya hiyo.
Aidha hii ya viunganishi husababisha barabara kadhaa zinazoleta magari mengi kwa wakati mmoja kwahusu machache tu kuondoka na hivyo kufanya msongamano mkubwa. Kwa kuwa kila gari lazima isubiri gari lililo katika mzunguko liondoke.
Aidha viunganishi vingine ni vile ambavyo barabara yingi huunganishwa na kuruhusiwa kwa kutumia taa za barabarani. Mfano wa viunganishi hivyo ni vile vya mataa ubungo, magomeni, foire, mwenge, tazara Daraja la Sarender, na Morocco. Katika aina hii ya viunganishi kama ilivyo katika viunganishi vya mzunguko magari mengi huja na machache tu huruhusiwa. Kiukweli hapa huwa ni hatari zaidi.
Jambo jingine linalochangia ni mwelekeo wa vituo vya magari. Katika hili angalia kituo cha mabasi mbezi mwisho, mtaa wa Congo, Msimbazi na Posta mpya. Baadhi ya vituo nilivyovitaja havijachepushwa pembeni ya barabara rasmi ili kuruhuru magari mengine yanapo shusha abiria mengine yaendelee bila kikwazo. Na sehemu nyingine kama mchepuo upo ni mdogo sana haukidhi mahitaji. Nauliza wataalamu wetu wapo wapi?
Vingine vilivyo chepushwa vizuri kama ubungo na mbezi mwisho tatizo hutokea pale magari hayo yanapo rudi katika barabara kuu. Yanaporudi hasa pale kama yanarudi mjini huzuia magari mengine hasa ukizingatia ni mlimani foleni huwa kubwa.
Matuta haliyojengwa huongeza msongomano pia. Hoja inakuja kwani hakuna anayefikiria kujenga daraja kama la manzese kuondoa matuta ya Kimara yanayosababisha foleni? Je hakuna anaefikiri Magari kama pale mbezi yangevukia upande wa pili kwa kupita juu au chini?
Je katika matatizo ya foleni za katika mataa hakuna anaeona tatizo kuwa aina ya viunganishi ni tatizo? Kwanini ujenzi wa barabara za juu usiwe wa kipaumbele? Ninachosikia ulazima ni fire na Tazara tu. Vipi ubungo, buguruni Daraja la Sarender au Mwenge?
Suala kubwa ni mpangilio madhubuti wa barabara zenyewe. Katika hili barabara zinazozunguka jiji hazitoshi na kufanya foleni itamalaki. Aidha barabara zinazotoka katikati ya jiji (CBD) kwenda nje ya jiji nazo ni tatizo mfano endapo kungekuwa na barabara ya Old Bagamoyo, sinza na kigogo zimenyooka toka maeneo ya CBD hadi nje ya jiji maeneo ya Bahari Beach, Tegeta, Mbezi. Kinyerezi n.k foleni za Barabara za Morogoro, Samnojuma, Mandera, Uhuru na Nyerere zingepungua sana.
Kutokana na mpangilio mbovu wa jiji kufanikisha barabara za kuzunguka CBD na zile zinazotoka katikati ya jiji kwenda nje zingesababisha ubomoaji wa hali ya juu. Aidha tofauti Barabara usafiri wa Reli ambao haujapewa kipaumbele ni suluhisho kubwa la muda mrefu la msongomano katika majiji mengi duniani.
Nauliza haya kwa kuwa najua ongezeko la idadi ya watu ni kubwa sana. Jiji hili ni miongoni mwa majiji yanayokuwa kwa kasi. Tena bila mpangilio ni maafa hayo. Mipango hii ya zima moto itatufikisha wapi? Mie nauliza tu.